MWONGOZO WA MAPAMBAZUKO YA MACHWEO A COMPREHENSIVE STUDY GUIDE

MWONGOZO WA MAPAMBAZUKO YA MACHWEO (STUDY GUIDE)

UTANGULIZI
Mwongozo huu una nia ya kuwa mwanga gizani kwa wasomi wa diwani ya ‘Mapambazuko ya
Machweo na Hadithi nyingine, kwa kutoa maelezo maridhawa kuhusiana na hadithi tofauti
zilizomo humu. Ili kufanikisha hili, mwongozo huu umeangazia masuala kadhaa katika hadithi.
Kabla ya kwenda katika hadithi binafsi, ni vyema kuangazia vipengele Fulani vya diwani.
MADA: Mapambazuko ya Machweo.
Mada ya diwani za hadithi fupi huwa ni mada ya mojawapo wa hadithi zilizomo. Hata hivyo,
sharti iwe mada ya kuvutia wasomaji na pia yenye kubeba uzito katika diwani husika. Lnafaa
kuwa mada ambayo ina uzito wa kutosha kubeba ujumbe wa diwani.
Mada ‘Mapambazuko ya Machweo’, ina athari ya kipekee kwa msomaji. Mapambazuko ni
majira ya alfajiri, kabla ya jua kuchomoza hali Machweo ni wakati wa jioni, jua linapotua.
Ukinzani katika mada unazua taharuki kwa msomaji, ambayo inamtuma kupitia hadithi za diwani
hiyo ili kufahamu vipi Mambazuko yanatukia wakati wa Machweo.

Mada hii inaleta fikra tofauti. Kwanza, ujumbe wake unaweza kurejelea hali ya mafanikio baada
ya tabu tele. Isitoshe, majira haya yananweza kurejelea umri, mapambazuko yakirejelea ujana
nayo machweo uzee. Inaweza pia kumaanisha mafanikio katika machweo ya maisha(uzee).
Mada hii, hivyo basi, inabeba taarifa muhimu kwa ajili ya diwani nzima. Suala la matumaini au
mafanikio katika/baada ya taabu limesawiriwa katika hadithi nyingi kwenye diwani hii. Hivyo,
tunaweza kusema mada hii imefumbata ujumbe wa diwani nzima. Mifani ya hadithi
zinazodhihirisha hali ya ‘Mapambazuko ya Machweo’ ni kama’Mapambazuko ya Machweo’,
‘Fadhila za Punda’, ‘Toba ya Kalia’, ‘Nipe Nafasi’,
‘Ahadi ni Deni’, ‘Sabina’ na nyinginezo.
Hivyo basi, ni wazi kwamba mada ‘Mapambazuko ya Machweo’ inafaa kabisa kwa diwani hii.
JALADA:
Jalada katika diwani ya hadithi fupi aghalabu hubeba ujumbe wa hadithi iliyobeba anwani. Hali
si tofauti katika diwani hii. Jalada linaakisi hali katika hadithi ya ‘Mapambazuko ya Machweo.
Kuna bwana aliyevaa suti ambaye anaingia kwenye gari. Haikosi huyo ni Makutwa, anayemiliki
gari la kibinafsi pekee mjini Kazakamba.
Kando yake, kuna mwanamume na mwanamke wanaoonekana kuwa katika hali ya majibizano
kwa jinsi walivyoinua mikono, mwanamume mkono wa kulia na mwnamke mkono wa kushoto

nyuso zikielekeana. Hawa bila shaka ni Makucha na mkewe Macheo ambao wana mjadala mara
kwa mara kuhusiana na suala la Makutwa kumkebehi Makucha.
Kando ya wawili hao pembeni kulia, kuna kimeza kidogo chenye vifaa fulani na kiti chake.
Haikosi hapo ni sehemu anapouzia vitafunio Makucha. Pembeni kulia kulia nako kuna sehemu
ya nyumba, ambayo itakuwa ya Makucha na mkewe Macheo.
Mbele yao mbali kidogo, kuna watoto wadogo wanaoonekana kuwa katika shughuli za kuzoa
mchanga. Hawa ni watoto ambao Makutwa anawatumikisha katika mgodi wake kinyume cha
sheria.
Hali ya anga inadhihirisha kwamba ni wakati wa machweo. Kuna jua ambalo linaelekea kutua na
anga imetamalaki rangi ya samawati. Mchanga walikokanyaga wahusika wote unatuhakikishia ni
mandhari ya mji wa Kazakamba.
Kuutumia Mwongozo.
Mwongozo huu umechambua kila hadithi kwa mapana na marefu. Umeangazia masuala tofauti
tofauti katika hadithi zote, ili kuhakikisha kwamba maomaji anaelewa yanayoshughulikiwa kwa
ubainifu wa kipekee. Masuala haya yanaanzia kwa mtiririko wa hadithi na ufaafu wa anwani hadi
mitindo ya uandishi. Masuala yaliyoshughulikiwa ni pamoja na;
Dhamira ya Mwandishi.
Ni lengo la mwandishi, yaani sababu ya kuandika hadithi husika. Inaeleza ujumbe ambao
mwandishi alinuia kupitisha kwa msomaji. Inaweza pia kuelezwa kama mafunzo ambayo
msomaji anapata kutokana na kusoma hadithi husika. Dhamira inaweza kuwa kupitisha ujumbe
kwa njia tofauti ikiwemo kuonya, kusawiri hali Fulani katika jamii au kuelimisha kuhusu suala
fulani.
Maudhui
Ni masuala nyeti yanayoshughulikiwa katika hadithi. Ni mambo makuu hasa kuhusu jamii
yanayoibuka kutokana na kusoma hadithi Fulani. Baadhi ya maudhui yanayojitokeza katika
hadithi nyingi ni pamoja na elimu, utamaduni, mapenzi na ndoa, migogoro na migongano, uzinzi,
ulaghai na unafiki, usaliti, nafasi ya mwanamke, ubabaedume na mengi mengine.
Wahusika
Ni watu au viumbe ambao wanatumiwa na mwandishi kuwasilisha ujumbe wake kwa hadhira.
Katika hadithi zote, wahusika waliotumika ni binadamu, wanaoakisi jamii halisi. Wahusika hawa
hutofautiana kwa hulka(sifa) kulingana na ujumbe toofauti ambao mwandishi anawatumia
kupitisha. Hivyo basi, kila mhusika, wahusika wakuu na wasaidizi huwa na sifa zake na
umuhimu katika hadithi.

Mbinu za Uandishi.
Ili kuleta mvuto, mwandishi hawezi kutumia lugha iliyo kavu. Lazima aifinyange lugha na
kuisuka kipekee ili kuleta mnato kwa msomaji anapoanza kupitia kazi yake. Kuna aina tofauti za
mitindo ya uandishi ambayo hutumika kutimiza hili.

Print Friendly, PDF & Email
people found this article helpful. What about you?

0 0 votes
Article Rating
Subscribe
Notify of
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x